Saturday, 5 March 2016

SIKU YA WAPENDANAO ASILI YAKE.......


SAINT VALENTINE
http://www.habarileo.co.tz/images/resized/images/frequent/valentino_210_120.jpg







RANGI nyekundu, maua, mishumaa, alama za moyo, mitoko na mambo mengine ya mapenzi ndio yanayotawala mwezi huu na hasa leo katika Siku ya Valentine, inayoadhimishwa kuwa ndiyo Siku ya Wapendanao kwa maana ya mapenzi ya watu wawili; mwanamume na mwanamke.
Hata hivyo, historia ya Siku yenyewe ya Wapendanao, wala si kwa namna inavyoadhimishwa kuwa siku ya mapenzi hayo ya wapenzi wawili;
mwanamke na mwanamume. Fadha Frank O’Gara wa Kanisa la Whitefriars Street la Dublin, Ireland, anaelezea habari ya mtu ambaye ndiye chimbuko la siku hiyo, Mtakatifu Valentine, ambaye inaelezwa kwamba mabaki ya mwili wake yamehifadhiwa katika kanisa hilo.
Fadha O’Gara anasema Mtakatifu Valentine alikuwa Padre wa Kanisa Katoliki, aliyeishi katika karne ya tatu AD, wakati wa utawala wa Roma wa Claudias. Claudias inaelezwa kwamba alikataza vijana kufunga ndoa, kwa kuwa aliamini kuwa vijana ambao hawajaoa, ni askari wazuri na walikuwa wapiganaji wazuri, kuliko vijana ambao wameoa, ambao siku zote ni waoga katika vita wakihofia familia na wake zao wataishije kama wakifa vitani.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa jamii aliyoishi Mtakatifu Valentine, ilikuwa jamii huru katika kujiamulia mambo yao, ambapo ndoa za wake wengi zilikuwa nyingi kuliko za mke mmoja, ingawa wengi wao walivutiwa na imani ya Kikristo iliyokuwa ikisisitiza ndoa ya mke mmoja. Pamoja na kuwepo kwa utamaduni huo, Kanisa Katoliki katika jamii hiyo, lilisisitiza msimamo wake kuwa ndoa ni jambo takatifu kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja katika maisha yao na hilo lilipaswa kuheshimiwa.
Kwa kufuata msimamo huo wa Kanisa, Mtakatifu Valentine, akitambua kuwa Claudias amepiga marufuku ndoa kwa vijana, alianza kushawishi vijana na kuwasaidia kwa siri kufunga ndoa ya mke mmoja kwa kufuata imani ya Kikristo. Inaelezwa kwamba Mtakatifu Valentine alifungisha ndoa mpaka za wanajeshi kwa siri, hatua iliyosababisha akamatwe, akawekwa gerezani na kuteswa kwa kufungisha ndoa kinyume na agizo la Claudius.
*Gerezani
Mtakatifu Valentine alipokuwa gerezani, simulizi zinaeleza kuwa alionesha baadhi ya miujiza kwa wafungwa wenzake na viongozi wa magereza. Moja ya miujiza, ulifanyika familia Asterius, aliyekuwa akisimamia kesi ya kutakiwa kuuawa kwa Mtakatifu Valentine, kutokana na kosa lake la kufungisha ndoa kwa siri kinyume na agizo la Claudius. Jaji Asterius alikuwa na mwanawe wa kike aliyekuwa na upofu, lakini kwa maombi ya Mtakatifu Valentine, mtoto huyo akapona, hatua iliyosababisha Jaji huyo kuwa Mkristo.
kumuombea Asterius akapona upofu , Valentine alihukumiwa huyo kwa kutumia Sheria Roma. Kukatwa kichwa Hukumu dhidi ya Mtakatifu Valentine, ilitaka achukuliwe hatua tatu za mateso; ya kwanza apigwe na maaskari, pili apigwe mawe na kisha akatwe shingo kwa sababu ya msimamo wake katika ndoa za Kikristo.
Inaelezwa kwamba baada ya kupokea hukumu hiyo, kabla haijatekelezwa Mtakatifu Valentine aliandika ujumbe wa mapenzi kwenda kwa mtoto wa kike wa Asterius, ambao mwisho ujumbe huo uliishia na neno; “kutoka kwa Valentine wako.”
Kuna taarifa kwamba Mtakatifu Valentine alimpenda kimapenzi mtoto huyo wa Jaji aliyemfunga, ndio maana aliandika ujumbe huo kwake. Fadha O’Gara akielezea mtazamo wake kuhusu Mtakatifu Valentine alivyokuwa, anasema kuna wakati mtu atalazimika kuonesha waziwazi anachoamini hata kama yuko karibu na kifo.
*Mabaki ya mwili wake
Mateso dhidi ya Mtakatifu Valentine, hayakuishia hewani kwani jamii mpaka leo inamkumbuka na Kanisa la Whitefriars Street Church, ni moja ya makanisa matatu yanayodai kwamba limehifadhi mabaki ya mwili wa Padre Valentine. Kutokana na madai hayo, leo hii watu wengi husafiri kwenda kuhiji katika kanisa hilo, kwa heshima ya kumbukumbu ya Mtakatifu huyo wa Kikristo.
“Sasa Mtakatifu Valentine anajulikana kama mlezi na Mtakatifu wa wapendanao. Kabla ya kuingia katika ndoa ya Kikristo, lazima uzingatie maandiko ya Mungu katika maisha yako...unahitaji uwezo wa Mungu katika maisha yako. “Kama Valentine angekuwepo hapa leo, ambacho angesema kwa watu walio katika ndoa, kwamba kuna wakati mtakabiliwa na majaribu na shida mbalimbali katika ndoa, kiasi cha kutishia kutunza kiapo chako cha ndoa.
“Lakini usishangae mapenzi moto moto uliyo nayo kwa mume au mkeo, yakabadilika na kupoa na labda kuanza kuingia katika maisha ya kiutu uzima hivyo ndoa changa, ziwe tayari kukabiliana na changamoto hizo,” anasema Fadha O’Gara. Anawataka wanandoa, siku ya ndoa yao kufikiria changamoto hizo,” anasema Fadha O’Gara na kuongeza kuwa; Mapenzi kwa wanadamu na mvuto wa kimapenzi katika ndoa ni mambo yanayopendeza na yaliyobarikiwa na Mungu, lakini katikati yake kuna kivuli cha msalaba, na hiyo ndio maana ya Valentine kwake.
*Sherehe duniani
Siku ya Valentine au Siku ya Mtakatifu Valentine, imekuwa ikisherehekewa kila Februari 14 ya kila mwaka. Ni siku ambayo watu huonesha mapenzi yao kwa watu wengine, si lazima wake kwa waume, bali hata wazazi, watoto na marafiki kwa kuwatumia kadi, maua au chocolates vikiambatana na ujumbe wa mapenzi.
Kuna baadhi ya jamii, wamejenga utamaduni wa kila miaka minne, Siku ya Wapendanao wanawake walioolewa hutoa tamko la kudumisha ndoa na mumewe. Pia kuna taarifa kwamba Siku ya Wapendanao, ni utamaduni wa Waroma uliokuwepo kabla ya Mtakatifu Valentine mwenyewe, ambapo kulikuwa kukifanyika sherehe.
Inaelezwa kwamba Waroma walikuwa na sherehe iliyoitwa Lupercalia iliyokuwa ikifanyika katikati ya kila Februari, wakati wa kuanza kwa majira ya joto. Katika sherehe hizo, wavulana walikuwa wakiletewa vikasha vyenye majina ya wasichana na kutakiwa kuokota karatasi na kutaja jina la msichana katika karatasi husika. Baada ya kutaja jina hilo, mvulana huyo alipaswa kuwa rafiki na msichana husika na wakati mwingine ukubwani, wako walioendeleza urafiki wao mpaka katika ndoa.
Inaelezwa kuwa baadaye, Kanisa lilidhamiria kubadilisha sherehe hizo kuwa za Kikristo na kuamua kuzitumia kumkumbuka Mtakatifu Valentine. Baadaye, jina la Mtakatifu Valentine, likaanza kutumiwa na jamii katika kuelezea hisia zao kwa watu wanaowapenda.
Kwa sasa siku hiyo ya Mtakatifu Valentine, imekuwa ikisherehekewa kila february 14 karibu dunia nzima, ingawa katika nchi na mataifa mengi ikiwemo Tanzania, inasherehekewa lakini si siku ya mapumziko, ingawa mwaka huu imeangukia siku ya mapumziko. Imetafsiriwa kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
By joseph Joachim
josejoachim01@gmail.com
http://thejoses01.blogspot.com/2016/03/siku-ya-wapendanao-asili-yake.html


No comments:

Post a Comment