JE HURUMA YAKO NI KAMA HURUMA YA MUNGU?
JUMAPILI YA 4 YA KWARESIMA
1. Yos. 5: 9a, 10 -12
|
2 Kor 5: 17-21
|
Lk 15: 1-3, 11-31
|
Kama kuna nguvu kubwa tuliyo nayo ni nguvu ya kuwa na sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Tuna DNA ya kiroho ya Mungu. Kwa nguvu hiyo tunaweza kuwa na huruma kama Mungu. Mungu haweki kando huruma yake, tusiweke kando huruma yetu. “Wingu jeusi siyo alama kuwa jua limepoteza mwanga wake; na hatia nyeusi sana siyo hoja za kusema kuwa Mungu ameweka kando huruma Yake,” alisema Charles Spurgeon. Baba wa wana wapotevu wawili hakuweka kando huruma yake, alimsamehe mwanampotevu aliyeenda nchi za mbali na kurudi. Mwanampotevu aliyebaki nyumbani aliweka kando huruma:hakumsamehe “Baba” na hakumsamehe kaka yake. Mhusika Mkuu katika kisa cha mwana mpotevu ni baba mwenye huruma.
1. MACHO YA HURUMA
“Baba yake alimwona angali mbali, akaona huruma” (Luka 15: 20).
Mt. Augustino alikuwa na haya ya kusema, “Kabla ya kumtambua baba akiwa mbali, wakati alikuwa anamtafuta, baba yake alimuona.” Macho ya Mungu ni macho yenye huruma, macho yanayoona, ni wa kwanza kutuona.
Kuna msichana wa miaka kumi na miwili alikuwa anakusanya pesa za kusaidia watoto wenye shida. Alimwendea meneja wa benki kuomba msaada. Meneja kabla ya kumsaidia alimuuliza kama anaweza kungundua kati ya macho yake mawili ni lipi jicho la bandia. Mtoto baada ya kuangalia macho ya meneja kwa umakini mkubwa alimwambia jicho lake la kushoto ni bandia. Meneja alitaka kujua mtoto huyo alijuaje. Mtoto huyo alisema: “Jicho lako la kulia linatazama kwa huruma. Hilo siyo jicho bandia.” Ni kama mtoto huyo alikuwa anasema: Jicho ambalo halina huruma ni jicho bandia.
Jicho la huruma tunaliona mwili wa marehemu unapoagwa. Kuna ambao wanajicho la huruma waonapo ombaomba, maskini, mgonjwa, mwenye njaa, mwenye huzuni, mwombolezaji, mfiwa, yatima, mjane, mgane, mwenye ulemavu kutaja aina chache za watu. Lakini kuna watu wenye macho ambayo si mazuri: jicho ovu, jicho la dharau, jicho la kumcheka mtu, jicho la uchoyo, jicho la hasira, jicho la uasherati, jicho la wivu au jicho la husuda, na jicho la chuki.
Katika sala ya huruma ya Mungu ya Papa Francis tunasali hivi: “Jicho lako lililosheheni upendo lilimwokoa Zakayo na Mathayo waliokuwa watumwa wa fedha; lilimwokoa mwanamke mzinzi na Magdalena aliyekita furaha yake kwa kiumbe; ulimfanya Petro aangue kilio baada ya uasaliti; ukamhakikishia Paradiso, mwizi aliyetubu. Tuwezeshe kila mmoja wetu kusikiliza lile neno ulilomwambia mwanamke Msamaria: kama ungetambua zawadi ya Mungu.”
Jicho la huruma ni jicho la kuelekeza. Bwana wetu Yesu Kristo alimwelekeza kwa jicho Mtume Petro. Alimkonyezea kutoka nje, kupumzika na kujifikiria kidogo, na atagundua jambo alilolitenda. Tumia jicho la huruma kuwaelekeza watoto wako wanapokosa mbele ya wageni, wanapokosa adabu mbele ya wageni, waelekeze watoke nje. Jitahidi kuwa na macho ya huruma.
2. MIGUU YA HURUMA
“Alimkimbilia” (Luka 15: 20)
Miguu ya huruma ni miguu inayoenda haraka kusaidia, kuhudumia, kutoa msaada. Moyo ulipolalia ndipo miguu huamkia. Ni methali ya Tanzania. Miguu ya huruma inatokana na moyo wa huruma. Mtu mwenye miguu ya huruma wahaya humuita: BIGURU BINTIRIMBIRA. “Baba yake alimwona angali mbali, akaona huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia, akambusu” (Luka 15: 20). Mt. Ambrose alisema, “Anakimbia kukutana na wewe, kwa sababu anakusikia unapotafakari siri za moyo wako na ulipokuwa mbali alikukimbilia hili mtu yeyote asimzuie.” Katika hadithi ya Mwanampotevu Baba mtu alimkimbilia. Hapo tunaona miguu ya huruma. “Tunasoma kuwa baba yake alikimbia. Hatua za kutubu ni za polepole, lakini miguu ya msamaha ni myepesi. Mungu anaweza kukimbia pale ambapo tunachemea taratibu, na tukiwa tunachechemea tunamwelekea yeye, atatukimbilia,” alisema Mchungaji Charles Spurgeon. Alipokuwa anakimbia bila shaka alikuwa anapungukiwa na pumzi lakini hakupungukiwa upendo.
Mwanampotevu alitenda makosa kwa kuondoka, tunaona miguu isiyo na huruma. Ni kama alifikiria, “Baba nimesubiri muda mrefu ufe haufi, nipe urithi wangu.” Mwana mkubwa alitenda makosa kwa kukataa kuingia ndani wakati sherehe inaendela, hapo tunaona miguu isiyo na huruma.
Watumishi walialikwa kuwa na miguu ya huruma, “Upesi leteni joho maridadi” (Luka 15: 22). Maneno “upesi leteni” yanadokeza nguvu ya haraka, na miguu ya huruma. Hakuna kupoteza dakika kumrudishia hadhi mwana mpotevu. Bikira Maria alikuwa na miguu ya huruma: “Siku zile Maria akafunga safari, akaenda hima…”(Luka 1: 39).
Miguu ya Yesu ilipigiliwa misumali kutukumbusha makosa tufanyayo kwa miguu yetu kutokuwa miguu ya huruma: kuvuta miguu unapotumwa, kuchelewa kwenda mahali palipo na shida kutoa msaada. Umepewa habari msiba wakati wa kiangazi wewe umeenda wakati wa masika. Ni methali ya Tanzania. Mguu usio na huruma hukanyaga wengine. Hata ukikanyagwa samehe. “Msamaha ni manukato ambayo ua huacha kwenye kisigino kilicholikanyaga,” alisema Mark Twain.
3. MIKONO YA HURUMA
“akamkumbatia” (Luka 15:20)
Mikono ya huruma ni mikono inayokumbatia. Mikono yetu ni mirefu kuweza kumkumbatia mtu walau hata shingoni. “Nguvu za mtu hazionekani katika nguvu za mikono yake. Zinaonekana katika upendo ambao kwao anakukumbatia,” alisema Steve Maraboli. Katika Biblia kuna kisa cha mwanampotevu aliyeomba urithi kutoka kwa baba yake akaenda na kutapanya hovyo mali kwa maisha ya anasa. Alipoishiwa aliamua kurudi nyumbani. Baba wa mwanampotevu alimkumbatia mwanae kwa mikono yenye upendo. “Baba yake alimwona angali mbali, akaona huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia, akambusu” (Luka 15: 20). Baba alimkumbatia mwanampotevu. Mikono yenye huruma ni mikono inayokumbatia mkosefu. Kuna methali ya kiafrika isemayo kuwa: mtoto ni kama shoka hata kama inakuhumiza , bado unaibeba begani. Kuna watoto ambao kama shoka wamehumiza wazazi wao. Lakini bado wazazi wananyosha mikono yao kuwakumbatia na kuwabeba. “Nilikuwa na rafiki wengi wa kunisaidia kuanguka; lakini katika kuinuka tena, niliachwa peke yangu, mpaka nashangaa kuwa kila mara sikuwa chini. Namsifu Mungu kwa huruma Yake; ni yeye peke yake aliyenyosha mkono na kunivuta. Abarikiwe daima! Amina” - Mtakatifu Teresa wa Avila
Mtakatifu Augustini katika tendo la baba kumkumbatia mwanampotevu aliona picha ya Yesu. Aliandika, “Mkono wa Baba ni Mwana.” Mkono wa Mungu baba wenye huruma ni Yesu. Kumbatio la Baba kwa wanadamu waliotenda dhambi lilikuwa huko Kalvari Yesu alipotufia msalabani. Kumbuka Yesu ni Sura ya huruma ya Mungu Baba. Baba wa Kanisa Ireneus alisema, “Mwana na Roho Mtakatifu ni mikono miiwili ya Baba.” Tunaweza kusema Mwana ni mkono wa huruma wa Mungu Baba na Roho Mtakatifu ni mkono wa huruma wa Mungu Baba. Mikono ya Mungu ni mikono ya huruma. Mikono ya Yesu ni mikono ya huruma. Katika mahubiri yake ya tarehe 4 Novemba 2013 Papa Francis alikuwa na haya ya kusema, “Dhambi zetu zipo katika mikono ya Mungu; mikono hiyo ya huruma, mikono iliyo na vidonda vya upendo. Haikuwa bahati mbaya kwamba Yesu alinuia kubaki na makovu katika mikono yake kutuwezesha kujua na kuhisi huruma yake. Hii ni nguvu yetu, matumaini yetu.” Kanisa Katoliki husali katika maombi Jumapili ya nne ya Kwaresima, “Utunyoshee mikono yako na kutuokoa tunapozama katika makosa na dhambi.” Mikono ya Mungu ni mikono inayookoa.
Mikono ya huruma ni mikono inayotoa. Mkono utoao ndio upatao. Ni methali ya Uganda. Inamaanisha kuwa mtu anayewapa wenzake vitu kwa ukarimu ndiye anayepokea tena kutoka kwao au kutoka kwa Mungu. Kutoa ni moyo vidole huachia. Ni methali ya Tanzania. Mikono inahusika katika kutoa. Kuna mwanadarasa aliyekuwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa, aliyeniambia hivi: “Ukija kwangu utakuta mlango nimesogeza kidogo ufungue kwa miguu.” Nilimuuliza, kwa nini nifungue kwa miguu?” Alinijibu, “Mikono yako itakuwa imebeba zawadi.” Mikono ya huruma ni mikono inayobeba zawadi, ni mikono inayotoa.
Mwanampotevu alimuomba baba yake urithi. “Mdogo akamwambia baba yake, “Baba, nipe sehemu ya mali iliyo haki yangu” (Luka 15:12). Baba yake alimpa urithi: “Basi baba akawagawia mali” (Luka 15: 12). Katika utamaduni wa kiafrika, mali inagawanywa baada ya kipindi maalumu cha maombolezo. Kutoa ombi kama hilo kungelisababisha hasira ya baba ambaye angelidhani kwamba mwana wake anatamani yeye afe (Rejea Hes 36: 7-9; Ybs 33: 19-23). Zawadi hizi ni alama ya ufahari wa papo kwa papo wa baba. Joho ni alama ya hadhi (Mwanzo 37:3). Pete ni alama ya mamlaka na alama ya kurejeshwa upya kwenye familia (Mwanzo 41:41). Viatu vinaashiria uhuru wa kijana. Watumwa na wanaotubu tu walitembea miguu wazi (2 Samweli 15:30). Mtakatifu Augustini alisema, “Kanzu zuri sana ni hadhi ambayo Adamu alipoteza; watumishi wanaoleta vazi ni wahuburi wa upatanisho.” “Wanawapotevu wanaporudi mambo makubwa yanafanyika,” alisema A.A. Dowty.
Tunaweka katika matendo tendo la huruma la kutoa tunapotoa sadaka. Kutoa sadaka ni tendo la huruma. Tunapowasaidia wenye shida ni tendo la huruma. “Upendo unafananaje? Una mikono ili kuwasaidia wengine,” alisema Augustine wa Hippo Afrika ya Kaskazini (354-430).
Mikono ya huruma ni mikono inayopokea. Kukataa zawadi nzuri ya mtu yenye kuzingatia vigezo vya kimaadili ni jambo baya. Kuna hadithi juu ya Ikengya ambaye walitaka kumpa glasi ya maziwa akasema, “Rusha.” Akaambiwa si maziwa yatamwagika. Akajibu, “Kwani anayekataa hukataaje?” Mwanampotevu alipokea mali kutoka kwa baba yake. Kikubwa alipochinjiwa mwana ndama, na kupewa pete, kanzu na viatu alivipokea.
4. SIKIO LA HURUMA
Baba (kama Mungu Baba) alisikia aliyofikiria, “Akajifikiria akasema, ‘Vibarua wangapi wa baba yangu wana chakula tele, nami ninakufa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, “Baba nimekosa mbele ya Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa tena mwana wako; unitendee kama mmoja wa vibarua wako” (Luka 15: 17-19).
Sikio lenye huruma ni sikio linalosikiliza. “Sala zetu na huruma ya Mungu ni kama ndoo mbili kisimani; moja inapotelemka nyingine inapanda,” alisema Mark Hopkins. Sala ikitelemka kwenye kisima cha huruma ya Mungu, huruma ya Mungu inapanda. Baba wa mwana wa mpotevu alimsikiliza mwanampotevu, alisikiliza alichokisema na ambacho hakusema kilichokuwa kinaendelea katika maisha yao. Baba alimsikia mwana mpotevu wakati anajifikiria, “Akajifikiria akasema, ‘Vibarua wangapi wa baba yangu wana chakula tele, nami ninakufa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, “Baba nimekosa mbele ya Mungu na mbele yako. Sistahili tena kuitwa tena mwana wako; unitendee kama mmoja wa vibarua wako” (Luka 15: 17-19).Mtakatifu Yohane Krisostomu alisema, “Sasa baba akitambua toba yake hakungoja kupokea maneno ya kutubu kwake, lakini alitarajia maombi yake ya unyenyekevu na alimwonea.”
5. MOYO WA HURUMA
“Baba yake alimwona angali mbali, akaona huruma (Luka 15: 20).
Hapa kuna moyo wa huruma. Moyo wazi mlango wazi. Nyumba haikosi nafasi kinachokosa nafasi ni moyo.Moyo wa baba wa mwanampotevu ulikuwa moyo wa huruma.
Mtu aitwaye Alice James mke wa William James alisimulia kuwa jioni mme wake alitoa maneno kama haya: “Yaani hatuwezi kukaa peke yetu walau jioni moja bila wageni. Lazima tuzungumze na watu kila jioni?” Mke wake alitoa jibu kama hili: “Nitajitahidi kuhakikisha anayepiga simu namwambia kuwa utakuwa na shughuli nyingi jioni.” Kwa hiyo wanandoa hawa walijaribu kutulia na msimamo huu. Lakini mtu alipobisha hodi mwanamke huyu alijaribu kwenda kumwambia mgeni kuwa mme wake ana shughuli nyingi. Cha kushangaza wakati anafikia mlango kabla ya kutoa maneno hayo mme wake alikuwa nyuma yake akisema kwa sauti ya juu kwa mgeni. Karibu ndani! Karibu ndani! Moyo wazi unahakikisha mlango huko wazi. Moyo wa ukarimu kwa wageni unahakikisha mlango huko wazi kwa wageni.
6. MIDOMO YA HURUMA
akambusu” (Luka 15: 20).
BY FR.FAUSTIN KAMUGISHA
No comments:
Post a Comment