1. UPENDO AGAPE
- UPENDO WA MUNGU. (Godly Love)
Agape
ni aina ya upendo wa ki-Mungu, utendao
kazi ndani ya mtu pasipo masharti yoyote au sababu yoyote. Ni upendo
usioangalia hali ya
nje ya mtu. Ni nguvu
au uwezo wa mvuto wa Ki-Mungu utendao kazi ndani ya mtu, kumwonyesha mtu
mwingine wema wa Mungu bila kujali hali yake yoyote. Ni upendo usio na sababu
yoyote; unampenda mtu kwasababu tu unatakiwa kumpenda, nukta. Hakuna sababu
nyingine. Kwa kingereza wanasema unconditional
love.
Aina
hii ya upendo; agape, ni kama ule aliotuonyesha Mungu kwa kutupenda. Neno la
Mungu linasema ‘Mungu alitupenda tungali wenye dhambi’ (Rum 5:8) ili atuokoe na
mauti itokanayo na uasi kwa Mungu. Imeandikwa katika biblia kwamba Mungu
aliupenda ulimwengu wenye kila aina ya uovu, uasi na uchafu (Yoh 3:16, Rum
1:28-32) na akamtoka Kristo afe kwa ajili yetu, ili tuokolewe. Kwahiyo,
alitupenda bila kujali uchafu na uasi tuliokuwa nao. Huo ndio upendo
wa agape.
Mfano; Upendo wa Msamaria mwema. (Luka
10:29-37)
Msamaria
mmoja alimkuta mtu mmoja asiyemfahamu, ameanguka barabarani kwasababu amepigwa
ma majambazi. Huyu Msamaria aliamua kumsaidia huyu mhanga kwa kumsafisha
vidonda vyake na kumchukua katika punda wake na kumpeleka katika nyumba ya
wagonjwa na si hivyo tu, bali alijitolea hata kumlipia gharama za matibabu, kwa
huyu mtu asiyemjua kabisa. Huu ndio upendo wa ki-Mumgu ndani ya mtu. Hauangalii
hali ya nje wala hauna masharti; bali mtu huamua kuuachilia tu kwa mtu,
kawasababu Mungu ameumimina ndani yake kwa ajili ya mtu/watu wengine.
Lakini
tunasoma kuwa, kabla ya huyu Msamaria kupita pale njiani na kumwuoka huyu
mhanga, walipita watu wengine wawili ambao wanaaminika kuwa ni watumishi wa
Mungu. Kwanza alipita kuhani wa Mungu, lakini hakutaka kumsaidia, labda
kwasababu hamjui. Neno linasema, alijipitisha kando akaenda zake bila
kumsaidia. Kisha akapita Mlawi, amabye pia ni mtumishi wa Mungu, lakini naye
pia alijipitisha kando kabisa, akaenda zake bila kutoa msaada kwa huyu mtu,
kwasababu tu ni mtu asiyemfahamu. Pamoja na udini waliokuwa nao, tunasoma kuwa,
hawakuweza kumsaidia huyu mtu aliyejeruhiwa vibaya na majambazi. Ni aidha,
hawakuwa kabisa na upendo agape ndani
yao, au hawakuuachilia upendo agape utoke,
uhudumie mtu.
Lakini
cha kushangaza, akaja Msamaria (amabye ni mtu wa kabila lisilohesabika kuwa la
wacha Mungu) ndiye aliyeweza kuuruhusu upendo wa Mungu wa agape umhudumie yule mhanga wa ujambazi japo hamjui kabisa.
Akamsafisha viWale watumishi wa Mungu walishindwa kuuruhusu upendo agape kutoka ndani yao, kumhudumia huyu
mhanga. Hawa watumishi wa Mungu tuliowasoma, walitawaliwa na upendo wenye
masharti na unaoangalia kwanza hali ya nje ya mtu. Upendo agape hautakiwii kuangalia hali ya nje ya mtu, wala hautakiwi kuwa
na masharti yoyote. Ni upendo wa Mungu mwenyewe alitumiminia mioyoni mwetu kwa
uwezo wa Roho Mtakatifu (Rum 5:8)
Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa ki-Mungu
(Agape).
i.
Hauangalii hali
ya mtu ya nje.
ii.
Hauna masharti
yoyote ya kupenda.
iii.
Hauna kipimo au
kiwango cha kupenda.
iv.
Hauna mwisho au
kikomo cha kupenda.
2. UPENDO
PHILEO – UPENDO WA KIRAFIKI. (Friendship Love)
Phileo
ni upendo wa kirafiki. Huu ni
pendo tofauti kidogo na upendo wa agape.
Phileo ni upendo wenye sababu. Kiingereza wanasema ‘conditional love’. Ni upendo wenye sababu. Huu ndio upendo
unaokuwepo kati ya marafiki. Phileo ni
upendo unaoshikiliwa na kishikizo/kifungo cha ‘masharti’ fulani au ‘sababu’
fulani. Mtu huwa rafiki wa mtu fulani
‘kwasababu’ fulani. Kuna mazingra yamewafanya watu fulani kuwa marafiki.
Mazingira hayo au mashrti fulani yakivunjika kati yao, basi upendo ulio kati
yao huyeyuka na urafiki wao huvunjika.
Aina
hii ya upendo wa phileo ni kama ile
ambayo Yesu anaisema katika kitabu cha Yohana 14:21,23. Anasema kwamba ‘mtu akinipenda, Baba atampenda, nami na Baba
tutakuja kufanya makoa ndani yake’. Huu ni upendo tofauti na ule unaotajwa
katika Yohana 3:16 na Warumi 5:8 ambao unasema Mungu alitupenda tungali wenye dhambi pasipo masharti yoyote. Yaani, kwa upendo
agape, Mungu hakujali hali zetu za
nje wala masharti yoyote. Lakini kwa upendo
phileo, Mungu anaangalia kwanza kama mtu atatimiza masharti aliyoyaweka,
kisha ndipo na yeye Mungu anaachilia
upendo phileo kwa mtu huyo, anakuwa
rafiki yake.
Mahali
pengine Yesu alisema kwa wanafunzi wake kuwa ‘siwaiti ninyi tena watumwa bali marafiki.’ Hilo neno ‘tena’ linamaanisha kwamba, baada ya
kukaa na wanafunzi wake kwa muda fulani, waliweza kufikia kiwango Fulani cha masharti alichokitaka Bwana, hata sasa wamefika
katika ngazi wa kuwa marafiki wa Yesu na sio watumwa tena. Ndio maana imeandikwa
pia katika kitabu cha Mithali 8:17 kuwa, ‘ninawapenda wale wanipendao …’ Hivyo phileo ni upendo wenye masharti na
sababu. Rafiki wa mtu husema ‘nampenda mtu
Fulani, rafiki yangu kwasababu …’ Labda kwasababu wanasoma wote au kwasababu
alimsaidia katika eneo fulani au kwasababu anatabia fulani au kwasababu
wanatoka kijiji kimoja, n.k.
Mfano; Urafiki wa Jonathan na Daudi. (1Samweli
18:1-4)
Tunaona
Jonathan anampenda sana Daudi baada ya kugundua vipawa vilivyo ndani ya Daudi.
Tunasoma kwamba Daudi alikuwa anajua sana kupiga muziki (zeze) na kuimba zaburi
kwa Mungu, kitu kilichofanya Daudi awe karibu sana na Mungu na kufunikwa na
utukufu wa Mungu (upako). Hivyo Jonathan alimpenda sana Daudi kwasababu Daudi ana upako, uliomsaidia
babake (mfalme) Sauli kufunguka kutoka katika nguvu za giza mara kwa mara. Hivyo
Daudi akawa mtu wa msaada sana kwa familia ya Mfalme na katika serikali yake.
Pasipo Daudi kuwepo karibu, mambo yote ya ofisi ya Mfalme na nyumba yake
yanaharibika. Hicho kilimfanya Jonathan kumpenda sana Daudi. Na Daudi naye
akampenda sana Jonathan kwasababu Jonathan alimpenda yeye kwanza, na pia
kwasababu Jonathan alikuwa mototo wa mkuu wa nchi, mtoto wa Mfalme. Kukajengeka
upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Daudi na Jonathan, upendo Phileo. Hivyo, Phileo ni upendo wenye sababu au masharti.
Mfano Mwingine; Urafiki wa Yesu na
Lazaro, Mariam na Martha. (Yohana 11:5, 35-36)
Japo
biblia haielezi wazi wazi sababu za
urafiki wao, lakini maandiko yanaonyesha wazi kuwa, uhusiano wa Yesu na kina
Lazaro, Martha na Mariam, ulikuwa wa karibu sana ingawa hawakuwa ndugu zake
wala wanatimu wake, bali marafiki zake. Angalia inavyoelezwa katika msatri wa 5;
Neno la Mungu linasema, 5Naye Yesu alimpenda Martha na umbu lake
(dada yake, ambaye ni Mariam) na Lazaro (kaka yao). Hebu jiulize, kwanini Roho
Mtakatifu alimwongoza Yohana kutanguliza kumuandika Martha kwanza, kabla ya
Lazaro au Mariam? Hii ni wazi kwamba, Yesu alikuwa na uhusiano wa kirafiki,
tena wa karibu sana na hii familia, na hasa Martha (nionavyo mimi, kulingana na
maandiko). Tuangalie zaidi mazingira haya kama ilivyoandikwa.
Yohana
11:20; Martha aliposikia kwamba hatimaye Yesu amefika msibani japo kwa
kuchelewa, alikwenda kumlaki (kumpokea) lakini Mariam hakutoka, alibaki ndani.
Unadhani kwanini? Baada ya kuongea na Yesu kwa muda Fulani, ndipo tunamuona
Martha akiamua kwenda kumuita na Mariam, atoke ndani kwenda kumsalimia Yesu (mstari
wa 28-32) Hii inaonyesha ukaribu uliokuwepo kati ya Yesu na Martha. Walikuwa na
upendo mkubwa sana wa kirafiki, Phileo.
Wasomaji wa Biblia nakumbuka hata wakati Yesu alipotembelea familia yao siku
moja, ni Martha aliyeonyesha kumjali Yesu sana hata kujituma jikoni ili
kumuandalia chakula, wakati Mariam hakuwa hata na pressure, bali alijiketisha miguuni pa Yesu kusikiliza Neno la
Mungu. Japo badaye Martha alishushuliwa na Yesu, lakini ndiye aliyeonyesha
kumjali (kum-care) Yesu zaidi, ndiye
aliyeonyesha kusumbuka kwa ajili ya Yesu zaidi kuliko Mariam. Soma hii katika
kitabu cha Luka 10:38-42.
Mimi
naamini urafiki wa Martha kwa Yesu ulijengeka katika mazingira ya Martha kuthamini
wema na baraka alizotendewa na Yesu, kwasababu utakumbuka kwamba, Martha ndiye
yule mwanamke kahaba, ambaye siku moja alisikia injili katika mkutano ambao
Yesu alikuwa anahubiri na akatubu dhambi zake, akatua mzigo wake na
akamsamehewa kabisa uovu wake wote. Kwa furaha aliyokuwa nayo, akaenda nyumbani
kwake, akachukua chupa ya perfume
(marhamu) safi tena ya bei kubwa, akaja mahali ambapo Yesu alialikwa chakulani
nyumbani kwa Farisayo aitwaye Simon.
Kwa
utaratibu wa kiyahudi, ni mwiko kabisa mwanamke kuingia katika kikao cha
wanaume wala kumgusa mwanaume bila utaratibu. Lakini kwa jinsi alivyokuwa na
msukumo mkubwa moyoni, alishindwa kujizuia, akapenya mpaka mahali walipokuwa
wamekaa chakulani, akasimama nyuma ya Yesu, akadondosha machozi katika miguu ya
Yesu (kwasababu wayahudi hukaa chini kwenye zulia, na hii ina maana kwamba,
Yesu alikuwa amekunja miguu kwa nyuma, ndio maana machozi yakamwangukia
miguuni). Ndipo alipoinama na kuvunja
ile ya marhamu safi, nyumba yote ikajaa harufu nzuri. Martha akaipaka miguu ya
Yesu mafuta yale mazuri, akachukua nywele zake ndefu na kuipangusa vizuuuri
miguu ya Yesu. Mwisho akamalizia kwa kuibusu sana miguu ya Yesu mpaka mafarisayo
wakakwazika na kunung’unika; lakini Yesu akamtetea Martha na kusema ‘mwacheni!
Huyu amesamehewa dhambi nyingi kuliko ninyi, ndio maana amenipenda zaidi sana
kuliko ninyi wote. Kwa habari kamili, soma Luka 7:36-50.
Pengine
kwa sababu ya unyenyekevu wa Martha, ndipo upendo wa kirafiki (phileo) ulipozaliwa kati ya Yesu na
Martha. Tunasoma hatimaye siku nyingine, Martha akamualika Yesu chakulani
nyumbani kwao (Luka 10:38-42). Kitendo hicho kilimtabulisha Yesu kwa familia ya
Lazaro. Biblia inasema Yesu akawapenda sana Martha, Mariam na Lazaro kirafiki - phileo (Yoh 11:1-5). Baada ya
hapo, ndipo Lazaro alipougua sana hata Martha akatuma watu kwa Yesu kumwomba
aje kumponya kaka yao ambaye pia ni rafiki sana wa Yesu. Mpaka Lazaro anakufa,
Yesu alikuwa hajatokea.
Siku
Yesu anafika, walikuwa wameshamzika Lazaro siku nne zilizopita, tayari ananuka,
ameharibika. Habari ziliposikika kwamba Yesu amefika msibani, ni Martha peke
yake aliyetoka kwenda kumlaki Yesu. Baada ya muda, Martha kuongea na Yesu kwa
muda, ndipo akarudi ndani kwenda kumwita Mariam atoke kwenda kumsalimia Yesu
kule nje. Mariam akatoka, naye alipomwona Yesu, alilia kwa uchungu sana na
kujibwaga miguu pa yesu na kulalama ‘Yesu kama ungekuja mapema, kaka yetu
asingekufa, ungemponya’. Yesu alipomwona Mariam analia, na wayahudi
waliofuatana naye wanalia, Yesu akaugua sana moyoni, akafadhaika, na mstari wa
35 unasema “Yesu akalia machozi”. Hata wayahudi
walipomuona Yesu analia, wakasema, “angalia jinsi alivyompenda (Lazaro)”. Hii
inaonyesha kwamba, kulikuwa na upendo mkubwa sana wa kirafiki kati ya Yesu na
Lazaro na dada zake. Baada ya hayo, tunaona kwamba Yesu alienda kumfufua rafiki
yake Lazaro kutoka mautini.
Ndipo
katika sura inayofuata (Yoh 12:1-8) baada ya wakati fulani kupita tangu Yesu
amfufue Lazaro, tunaona familia ya Lazaro wanamwandalia Yesu karamu (sherehe au
party), pengine ilikuwa ni ibada ya shukurani ya kufufuka kwa Lazaro. Siku
hiyo, Martha akaanda chakula kizuri, halafu wote wakiwa wameketi chakulani,
Martha akarudia tena kumvunjia Yesu kibweta cha marashi safi, kumbuka hii ni mara
ya pili anamfanyia Yesu tendo hili la upendo.
Martha akamvunjia Yesu kibweta kingine cha marashi (perfume) safi ya bei kubwa;
akampaka tena Yesu marhamu safi kwa nywele zake. Ilikuwa ni ratili ya mafuta
safi ya marhamu yenye thamani nyingi. Safari hii Yuda ndiye aliyekwazika (soma
mwenyewe utajua sababu). Lakini tunamwona Yesu akimtetea tena Martha na kusema
‘mwacheni, kwa kitendo hiki, ananiandaa kwa maziko yangu’. Hii inatuonyesha
jinsi Yesu alivyokuwa na urafiki wa Karibu sana na Martha. Martha alimpenda
sana Yesu kwa wema usioelezeka, ambao Yesu alimtendea yeye na familia yake. Upendo
uliokuwa katikati yao ni upendo phileo,
Upendo wa kirafiki, upendo wenye sababu.
Sifa kuu tatu (3) za Upendo wa kirafiki
(Phileo).
i.
Unaangalii hali
ya mtu ya nje.
ii.
Una masharti
yoyote ya kupenda.
iii.
Una kiwango au
kipimo cha kupenda.
iv.
Una mwisho au
kikomo cha kupenda.
3.
UPENDO EROS – UPENDO WA KIMAPENZI AU MAHABA. (Romantic/Sexual
Love)
Eros ni upendo wa kimapenzi au kimahaba unaokuwa kati ya watu fulani kusababisha
watu hao kuwa na uhusiano wa kimapenzi (mahaba) kati yao. Kwa utaratibu wa
Mungu na jamii zilizo ‘sawa sawa’, Eros ni
aina ya upendo unaotakiwa kuwa kati ya watu wenye uhusiano wa ki-ndoa, yaani
mtu mke na mume au kati ya watu wanaoelekea katika uhusiano wa ki-ndoa wa mume
na mke. Aina zote za upendo zinahusisha moyo (nafsi) wa mtu, lakini Eros huwa na sifa ya kuwa na hisia zenye
nguvu zaidi toka moyoni kuliko aina zingine zote za upendo. Eros ni aina ya upendo wenye nguvu kali sana ya
hisia za binadamu.
Tunaona
Neno la Mungu (katika kitabu chake maalum kinachohusu mahaba ya wapenzi wawili) kitabu cha Wimbo Ulio Bora 8:6, Neno la Mungu linasema kwamba Upendo (Eros) huwa na nguvu
sana, kama mauti. Nguvu hiyo ya upendo huunganisha nafsi (fikra,hisia na
maamuzi) za wapenzi wawili kuwa kitu kimoja katika fikra, hisia na maamuzi yao
kwasababu ni upendo uliolenga kujenga ndoa nzuri na familia bora.
Mfano; Upendo wa Yakobo kwa Raheli. (Mwanzo
29:10-30)
Yakobo
alipomkimbia kaka yake Esau, alikimbilia nchi ya mbali, nchi ya mama yake, kwa
mjoba wake Labani. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo
waliitwa Raheli. Biblia inasema Lea alikuwa na macho mazito, yaani
ukimwangalia, utadhani amelala, kumbe ndio anakuona. Na Raheli alikuwa na umbo
zuri la mwili na sura nzuri ya usoni. Na Biblia inasema kwamba, Yakobo
alimpenda Raheli. (Mwa 29:16-20). Labani akamwabia Yakobo atumike kuchunga
wanyama wake kwa miaka saba (kama mahari), ndipo atampa Raheli kuwa mke wake.
Yakobo akapendezwa na hilo, na akakubali kutumika na kuchapa kazi za Labani kwa
miaka saba ili ampate Raheli. Na Neno la Mungu linasema, kwa jinsi Yakobo
alivyompenda Raheli (kwa Eros - kimapenzi
kuwa mke wake), alichapa kazi sana na kwa bidii kiasi kwamba, ile miaka saba
ilionekana michache sana.
Hiyo
ni nguvu ya upendo Eros. Yakobo
alikamatwa katika upendo eros kwa
Raheli. Ilikuwa kali sana. Nakwambia eros
ina uwezo wa kumfanya mtu asione ugumu wa kazi, asione machungu, asione
umbali wa mwendo, asione ukali wa jua, asione aibu wala woga mbele za watu
wengine; Eros ina nguvu sana juu ya
mtu mwenye nayo, hata kutawala utu wake wote. Eros ina nguvu ya fikra, hata kutawala mawazo ya mtu; eros ina nguvu ya hisia, hata kutawala
kuhisi/kujisikia kwa mtu; eros ina
nguvu ya maamuzi, hata kutawala matendo ya mtu kabisa. Unaweza ukamkuta kijana
siku hizi ni msaaaafi kuliko tunavyomjua, kumbe ni kwasababu tayari amekamatwa
kwa mwanamwali binti ‘Labani’ kama Yakobo alivyodakwa. Wee acha bwana!
Tehetehetehetehe (kicheko).
Yakobo
alijaa Raheli katika mawazo yake
yote! Kila saa alibaki kumuwaza Raheli kwa muda mrefu; Yakobo alijaa Raheli katika
hisia zake kiasi cha kutosikia
machungu ya ile kazi na hata akaona miaka saba kwa si kitu kikubwa; Yakobo
alijaa Raheli katika maamuzi yake
hata kumfanya afanye kazi kwa nguvu kama trekta au katapila, ili tu kumpata
Raheli. Raheli ndiye aliyekuwa nguvu na hamasa ya Yakobo kudamka alfajiri na
mapema kwenda kulisha mifugo ya mjomba wake Labani.Upendo Eros una nguvu kama mauti. Wee acha tu.
Upendo
wa kimapenzi au mahaba - Eros.
(Romantic Love or Sexual Love)
Upendo
wa kimapenzi huwa kati ya watu wawili wanaoelekea katika uhusiano wa kudumu wa
mume na mke. Mungu hakukusudia upendo huu wa kimapenzi uwe wa kujaribu na
kuacha, kwasababu eros ni upendo
wenye nguvu sana ya hisia (nafsi), hivyo huathiri sana moyo, ufahamu, hisia za
mtu na pengine hata afya ya mwili wa mtu kabisa, kama hatajua namna ya kuutawala
ipasavyo. Hivyo Eros si upendo wa
kuingia na kutoka utakavyo, kama mtu abadilishaye nguo (labda kama kuna cha
kujifunza; nitaeleza baadaye maana ya hii sentensi), bali eros ni upendo uliokusudiwa kukaa kati ya watu wawili tu,
kwa maisha yao yote yaliyobaki hapa duniani (permanently for life), sio kuingia
na kutoka, kwasababu una uwezo wa kujeruhi sana moyo wa mtu na kumwachia vidonda
na makovu ya moyoni. Tena nasisitiza, eros
ni kwa ajili ya watu wawili tu, na sio watatu au zaidi, laa sivyo
huo hautakuwa upendo, bali tamaa (lust and not love). Na tena eros, ni upendo kwa ajili ya watu wawili
wa jinsia tofauti tu, na sio jinsia moja.
Mfano; Upendo wa Isaka kwa mkewe
Rebecca. (Mwa 26:1-11)
Isaka
alikuwa akiishi katika nchi ya Wafilisti. Watu wale wakamwona Rebeka,
wakavutiwa na uzuri wake, hata wakamtamani. Wakamuuliza Isaka, ‘ee bwana ee,
huyu msichana tunayemwona katika boma lako na wakati mwingine unaambatana naye,
ni nani kwako? Isaka akaogopa kusema ni mke wake, kwa maana wangeweza kumuua
ili wamchukue Rebeka, kwa jinsi alivyokuwa mzuri wa kuvutia. Isaka akasema ‘ni
dada yangu’. Basi wakamwacha. Lakini kumbe wale watu walitumwa na Mfalme
Abimeleki, mfalme wa Wafilisti, ili kupeleleza na kujua uhusiano wao, kwasababu
Mfalme alivutiwa sana na uzuri wa Rebeka, akataka kumuao.
Siku
moja, Mfalme Abimeleki alipokuwa akiptia pita mitaani, akakatiza mtaa ambao
nyumba ya Isaka ilikuwepo. Biblia inasema
“8Abimeleki Mfalme akachungulia dirishani, akawona Isaka
akicheza-cheza na Rebeka mkewe” (kimahaba/romantically). Mfalme Abimeleki
akamwita Isaka, akamwambia, kwa jinsi nilivyowaona mnchezeana vile, haaaaata!
lazima huyu ni mkeo, huwezi kucheza-cheza vile na dadako, sasaaaa, mbona
uliniambia kuwa huyu ni ndugu yako (dadako)? Isaka akajibu ‘niliogopa nisije
nikauwawa kwa ajili yake’. Basi Abimeleki akamlaumu Isaka, kwa kusema, mtu
mmoja wetu angelala na Rebeka bila kufikiri ni mkeo, kwasababu ulisema mwenyewe
ni dadako. Ndipo Mfalme akaamuru watu wote wasimguse Isaka wala mkewe Rebeka;
akasema “11amgusaye mtu huyu au
mkewe, lazima atauawa”.
Baadhi ya Dalili na Sifa za Upendo wa Kimapenzi
(mahaba) - Eros (Romantic Love).
1) Mvuto kwa Haiba yake na kuchukuliana nayo. (Mwonekano
na tabia).
2) Kukaa mawazoni kwa mtu anayependa. (Kujaa moyoni)
3) Shauku kubwa ya kuwa pamoja kila wakati. (Kuambatana)
4) Heshima kubwa kwa mtu apendwae (Utii na Uaminifu)
5) Kumjali na kumtanguliza mtu apendwae. (Kipaumbele)
6) Zawadi na gharama kwa mtu apemdwae. (Kujitoa/Sacrifice)
7) Furaha na Amani kutawala moyoni. (Kuridhika)
Baadhi ya maandiko yanayotaja upendo eros. (Upendo wa kimapenzi)
(Waefeso
5:25.) Enyi waume, wapendeni wake
zenu kama Kristo alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake. (Mhubiri 9:8-9.)
8Mavazi yako yawe meupe siku zote; wala kichwa chako kisikose
marhamu. 9Uishi kwa furaha pamoja na mke umpendaye, siku zote za
maisha yako ya ubatili uliyopewa chini ya jua. (Wimbo Ulio Bora 7:1-10) 10Mimi
ni wake mpendwa (mpenzi) wangu na
shauku yake ni juu yangu. (Wimbo Ulio Bora 4:1-7) 1Tazama, u mzuri
mpenzi wangu, u mzuri, macho yako…nywele zako… 7Mpenzi wangu u mzuri
pia, wala ndani yako hamna hila.
4.
UPENDO STORGE – UPENDO WA KIFAMILIA. (Family Love)
Upendo storge ni upendo wa kifamilia, ni upendo unaotokana na damu moja ya
undugu. Ndugu wa damu moja hata kama hawapatani au wemegombana, bado ndani yao
kuna upendo wa kindugu. Fikiria; mtu na mdogo wake wakiwa wamegombana sana na
kutupiana mito ya makochi na vitabu vyote vya kwenye shelfu za kabati, baadaye,
mmoja akimkuta ndugu yake anaonewa au anagombana au anapigwa na muuza machungwa
wa mtaani, huyu ndugu yake kwa vyovyote ataguswa tu, ataonyesha kujali tu au
anaweza hata kuweka tofauti zao pembeni na kuingilia kumsaidia. Msukumo huo au
mvuto huo, ni mvuto unaotokana na viini vya upendo wa kifamilia
unaowafungamanisha watu wa damu ya familia moja au ukoo mmoja.
Mfano; Upendo wa Musa kwa Mwebrania
mwenzake. (Kutoka 2:11-12)
Musa
aliona mwebrania mwenzake akipigwa na mmrisri. Kwasababu na yeye alikuwa
mwembrania, ndani yake kukachemka mvuto wa kindugu, kuliwaka moto wa upendo wa
kifamilia. Akainuka na kwenda kumpigania. Musa akamuua yule mmisri na akamwokoa
yule mwebrania. Japo hawajazaliwa tumbo moja, lakini waote wana damu za
kiebrania, na viini vile vya asili yao, viliwafungamanisha katika pendo la
kindugu (kifamilia) hata wakasaidiana. Upendo huo ulimnyima Musa kujikausha
wakati ndugu yake anaonewa, anapigwa na anataka kuuwawa. Si ajabu wakati
anayatazama yale maonezi kwa mbali, hata alipojidai kuondoka bila kumsaidia, yamkini
miguu yake ilishindwa kutembea, nafsi yake ikakamatwa kurudi kumsaidia ndugu
yake. Hiyo ni nguvu ya upendo storge, upendo wa kindugu.
Mfano; Upendo wa Baba kwa Mwana mpotevu.
(Luka 15:11-32)
Tunasoma
jinsi mwana huyu mdogo wa baba tajiri alivyoomba sehemu ya urithi wake na
kutokomea nchi za mbali kwenda kutafuta maisha. Lakini maandiko yanaeleza jinsi
alivyovutwa na dunia na kuharibu mtaji wake wote wa mali alizopewa na
babaye.neno la Mungu linasema, kijana huyu alijiingiza katika anasa za dunia na
mwishowe alifilisika kabisa. Baada ya muda wa mahangaiko alipata kibarua cha
kulisha nguruwe wa mtu mmoja. Hali yake ya kimaisha ilikuwa mbaya sana hata
akatamani kula chakula cha nguruwe. Lakini akili zikamrudia na akaona anateseka
bure wakati kule kwao, baba yake ana watumishi wanaokula vizuri kuliko yeye.
Ndipo alipoamua kurudi nyumbani kwa toba. Kwa hali ya mzazi wa kawaida, huyu
kijana angepewa adhabu kali sana; lakini kinyume chake, baba yake mzazi
alimpokea kwa shangwe na furaha. Akamvika na mavazi mazuri, akamchinjia na
ng’ombe mnono na kumfanyia sherehe kuuuubwa ya kufana. Hiyo ni nguvu ya upendo
wa kindugu. Japo alichofanya si cha kupendeza, lakini nguvu ya upendo wa
kindugu unaweza kufunika uovu wooooote uliotendwa na ndugu yenu. Watu wanaweza
kuamua kusamehe au kufumbia macho makosa yaliyotendwa na ndugu yao kwasababu ya
nguvu ya upendo wa kindugu, unaitwa kwa kiebraia storge.
Upendo
wa kindugu, storge unafanana kwa sehemu na ule upendo wa ki-Mungu
wa agape.
i.
Hauangalii hali
ya nje ya mtu.
ii.
Hauna masharti ya
kupendwa.
iii.
Hauna kikomo au
mwisho wa kupendwa.
Tofauti
yake moja kubwa na upendo wa agape ni
kwamba, upendo wa kindugu una kiwango
au kipimo cho kupenda. Ndugu wanapendana lakini kwa viwango tofauti; upendo wao
haulingani. Tofauti ningine kubwa ni kwamba, kwasababu huu upendo wa kindugu unatokana na binadamu, basi ni
lazima hautakosa madhaifu mengi. Ingawa ndugu wanaweza kuwekeana masharti
fulani fulani ya kitabia ili kuweka uelewano kati yao, hata masharti hayo
yakivunjwa, na baadhi ya ndugu wakasema wamefika mwisho, hawataki tena
kumsaidia, lakini mwishoni, baada ya hasira kutulia na muda kupita, utaona
ndugu wanainuka, wanajikongoja, kwenda kumsaidia tu ndugu yao. Hiyo ndiyo nguvu
ya upendo wa kindugu au kifamilia.
NAMNA YA KUPATA MWENZI MZURI WA MAISHA.
(HOW TO FIND/GET A GOOD MARRIAGE PARTNER)
*Mithali
19:14, 21
1. Mweleze
Mungu vizuri, zile haja za moyo wako. (*Fil 4:6-7)
Mungu
ameahidi kuwa atakupa mtu wa kufanana na wewe (Mwa 2:18). Kwa hiyo ni muhmusana
ujijue wewe ukoje, kisha ndipo utaweza kumweleza Mungu na kumwomba akupe mtu wa
haja ya moyo wako. Hivyo ni muhiu sana kujijua, kujitambua na kujielewa kwa
jinsi ulivyo na ni aina gain ya watu ambao wewe unaendana nao (mnaiva). Hii ni
kwasababu, watu tuko tofauti. Unaweza kuishi na mtu yoyote duniani, lakini
hutaweza kuishi vizuri na kila mtu. Maisha mazuri yanakuja kwa kukutana na mtu ambaye mnaelewana na
mnaendana. Ndio maana Mungu alimwambia Adam kwamba, mwenzi wako wa maisha,
atafanana na wewe.
Usimfiche
Mungu moyo wako. Kumbuka, yeye ni Baba yetu na sisi tu watoto wake vipenzi.
Hivyo Mungu anaheshimu sana haja za moo wako ambazo zitakupa wewe furaha ya
maisha. Mathayo 7:7-11 inasema, Ombeni nanyi mtapewa. Mwana akiomba mkate,
hapewi jiwe, akiomba samaki, hapewi nyoka. Anapewa alichoomba. Lakini pia ni
muhimu ujue kwamba, mwana akiomba mkate, hapewi jiwe, lakini pia hapewi keki
hata kama ndani ya nyumba kuna keki. Mwana akiomba samaki, hapewi nyoka, lakini
pia hapewi kuku, hata kama ndani ya nyumba kuna kuku wengi. Hii ni kwasababu,
Mungu anaheshimu sana matakwa na mahitaji ya watoto wake, maana anapenda kuiona
furaha ya watoto wake. Soma Zab 145:17-18 na Isa 45:11 uone. Pia 1Kor 7:39.
Maombi
yako ya bidii yatampa Mungu kumchonga, kumuandaa. Kila mtu huumbwa na Mungu
vizuri, lakini Neno linasema kwamba, dhambi iliharibu utaratibu mwingi sana wa
Mungu duniani. Soma Mwa 6:5-8 na Rum 1:28-32. Dhambi imevuruga mambo mengi
sana, nafsi za watu wengi ziko corrupted (zimeharibiwa na kuvurugwa) na dhambi.
kwahiyo, maombi yako yatamfanya Mungu kuanza kumshughulikia na kumtengeneza
huyo mwenzi wako, popote alipo duniani. Na Biblia inasema kwamba, maombi ya
mwenye haki yanafaa sana, mt akiomba kwa bidii. Soma Yak :16,
Luk 18:1, Kol 4:2.
2. Mwombe Mungu
akuonyeshe au akukutanishe na mwenzi wako. (*Yer 33:3)
Kila
mmoja wetu ambaye Mungu amempangia kuwa na mwenzi, ana mwenzi huyo mahali
Fulani hapa duniani. Pointi ya kwanza inahusu kufanya maombi ya kumwmba Mungu
kumchonga na kumfinyanga huyo mwenzi wako popote alipo. Point hii ya pili
inahusu kumwomba Mungu kusababisha mazingira ambayo yatawakutanisha na
mtatambuana baada ya kupata ufahamu wa Mungu kwamba ‘you belong together’ yaani
mnaendana, mnafanana, mnafaana na hivyo mnaweza kuishi pamoja vizuri. Hiyo
ndiyo maana halisi ya kufunuliwa au kuonyeshwa. Japo Mungu anaweza kukupa maono
katika ndoto au katika maombi, lakini si lazima iwe hivyo. Si kila mtu anaweza
kupata maono kuhusu mwenzi wake. Soma Efe 1:15-19, Zab 32:8, Isa 43:26,
Isa 45:11
3. Tengeneza
marafiki. (*Mith 18:24, Mith 17:17)
Watu
wengi humwomba Mungu kwa uaminifu sana ili wapate mwenzi wa maisha. Lakini wanafanya
makosa ya kujifungia katika kisiwa cha upekee. Ni ngumu sana kuonekana na
kujulikana tabia na utu wako wa ndani kama hutachangamana na jumuiya za
marafiki. Mungu ndiye chanzo cha urafiki. Hata Yesu alikuwa na marafiki wa
kiume na wa kike pia. (Yoh 11:5).
Jithidi kufanya marafiki mbalimbali ila mwombe Mungu akupe marafiki
wazuri.
Kuna
aina nyingi za marafiki; Kuna marafiki wa mbali (peer friends), marafiki wa
kawaida (casual friends), marafiki wa karibu (close friends or best friends) na
marafiki wa moyoni (intimate friends). Unaweza ukawa na marafiki wa kawaida
wengi uwezavyo, haina shida. Lakini unahitaji marafiki wa karibu wachache (Mith
18:24). Katika wingu kubwa la marafiki zako, Mungu ataanza kukuongoza nawe
utawachuja na kuwaweka katika ngazi hizo mbalimbali. Katika hali ya kawaida,
Mungu atakukutanisha na mwenzi wako wa maisha kati ya marafiki zako na watu
unaofahamiana nao. Kwa maombi unayofanya, Mungu atasababisha mkutane,
mfahamiane, mtambuane na mpatane.
4.
Thibitisha moyo wako kwamba unampenda kikweli. (*Mhubiri 9:8-9a)
Kadri unavyoendelea na maisha ya uaminifu katika
wokovu, maombi, kujifunza neno la Mungu na kumtumikia Mungu kwa namna
mbalimbali, Mungu atasababisha ukutane na mtu anayefanana sana na haja za moyo
wako kuhusu mwenzi wa maisha. Utahitaji usikivu mkubwa wa rohoni ili kuambua ni
aina gani ya upendo unaingia moyoni mwako kuelekea kwake (kwasababu kuna aina
nne za upendo). Upendo wa Mungu, Upendo wa Kindugu, Upendo wa Kirafiki, Upendo
wa Kimapenzi (mahaba).
Katika ya watu unaofahmiana nao, yupo mmoja ambaye
atakuwa wa tofauti sana ndani yako. Mungu atampa kuonekana watofauti sana
kuliko wengine wote wanaokuzunguka. Hivyo kabla ya kwenda kusema naye na
kumshirikisha uonavyo wewe moyoni mwako, thibitisha kimaombi tena na tena
kwamba ndani yako kuna upendo wa kweli kwa ajli yake. Mk 5:25 – (30) – 34; inasema, wengi walimgusa
Yesu na kumsukuma-sukuma, lakini ni mmoja tu ambaye atakuwa na mguso wa tofauti
katika moyo wako.
ISHARA ZA KUTAMBUA (UPENDO WA) PENZI LA
KWELI.
1. Mtu huyo atakamata umakini wako na atakuvutia
(attention).
2. Atajaa moyoni na mwazoni mwako kuliko kawaida na
wengine.
3. Utatamani sana uwepo wake wakati wote (kuwa naye).
4. Utapenda kuwasiliana naye mara kwa mara (kama hamko
wote).
5. Utakuwa na moyo wa kumjali, wema, zawadi na kujitoa
sana kwa ajili yake.
6. Utakuwa na heshima ya juu sana, adabu, utii na
uaminifu sana kwake.
7. Utakuwa na maneno mazuri, maneno laini, na maneno ya
upendo kwake.
8. Utakuwa na moyo/uwezo wa kumvumilia au kuchukuliana
naye vile alivyo.
9. Utakuwa na hamu ya kumgusa au kumshika kwa upendo (si
tamaa).
10.
Utakuwa na moyo
na utayari wa kumlinda na kumhifadhi.
11.
Uhusiano wenu
utapendeza mbele za watu wengi (si lazima wote)
12.
Utakuwa na amani
na furaha ya ajabu moyoni mwako/mwenu.
Mungu alisema kwa mkono wa Mtume Paulo kuuelezea
Upendo kwa namna hii;
1
Cor 13 : 4-8(a)
*
Upendo huvumilia/subira (Love is patient)
*
Upendo
hufadhili/hufanya wema (Love is kind)
*
Upendo hauna
husuda (Love doesn’t Envy)
*
Upendo haujivuni
(Love is not proud)
*
Upendo haukosi
adabu (Love is not rude)
*
Upendo hauna
ubinafsi (Love is not selfish)
*
Upendo hauna
uchungu (Love is not easily angered)
*
Upendo hauhesabu
mabaya (Love doesn’t count wrongs)
*
Upendo haufurahii
uovu (Love doesn’t rejoice with evil)
*
Upendo hufurahia
ukweli (Love rejoices in truth)
*
Upendo unalinda
(love always protects)
*
Upendo huamini
yote (Love always trusts)
*
Upendo hutumaini
(Love always hopes)
*
Upendo
hustahimili (Love always perseveres)
5.
Omba ushauri kwa watu wanaokujua/wanaomjua huyo umpendaye.
2Kor 13:1;
Zab 73:24; Mith 15:22
Ushauri
kutoka kwa watu werevu wanaomjua Mungu na wanaowajua ninyi wawili
utakuhibitishia kwamba ulichsikia mooni juu ya huyo mtu ni sahihi. Wakati
mwingi (si wakati wote) watu wa pembeni huwa na uwezo wa kuona vizuri zaidi
mambo kuliko watu mlio ndani. Wanaweza kuona vitu ambavyo ninyi mlio ndani ya
urafiki hamuoni bado.washauri wanaweza kutumiwa na Mungu kuthibitisha mawazo
uliyo nayo na mipango uliyonayo. Mashauri ya watu yanaweza kukusaidia kufanya
maamuzi magumu nay a muhimu. (Math 18:16;
1Tim 5:19; Ebr 10:28)
Mwombe
Mungu akuongoze kwa watu wazuri wenye hekina watakaokushauri. Lakini la muhimu
kuliko vyote ni wewe mhusika kubaki na uamuzi wa mwisho. Washauri wabaki
washauri na sii waamuzi; wewe ndiwe uwe mwamuzi wa mwisho. Ni muhimu kupima
ushauri wote unaopewa kwa maombi na uongozi wa Mungu. Wakati mwingine, Mungu
anaweza kukuongoza kitu ambacho hakuna mtu mwingine anakiona ukionavyo wewe.
Neno la Mungu linasema, amani ya Kristo itakusaidia kufanya maamuzi mazuri.
Soma;
Fil 4:6-7, Kol 3:15 na Isa 55:12
6.
Mwendee na Useme naye kwa hekima.
(*Wimbo 3:1-4)
Baada
ya maombi na subira, Mungu akuongoze kusema naye kwa wakati utakaoongozwa na
Mungu. Uwe jasiri na muwazi. Lakini usemi wako uwe wa kawaida (simple).
Usichague maneno magumu wala misamiati wala mafumbo. Uwe wazi na wa kawaida.
Usitumie maneno ya kiroho saaaaana ili kumtisha au kumfunga mtoto wa watu. Kwa
mfano; usitumie maneno kama, ‘Mungu ameniambia’ au ‘Asema Bwana wa majeshi’
maneno kama haya, yanamfunga mtu kusema “ndiyo” (kama atashitushwa nayo na
kuogopa) lakini kama ni mtu jasiri na hajakupenda/hajakukubali, mtapambana. Huo
sasa si mwelekeo mzuri.
Kijana
mmoja alipoataliwa, akaanza kuporomosha maneno makali mfano ‘nakuzungushia
ukuta wa moto, hutaolewa na mtu mwingine ila mimi, na ukikataa, Bwana
atakutandika’. Hii si hekima ya Mungu. Mungu hatumii nguvu bwana. Ikiwa kwenda
mbinguni tuu, Mungu halazimishi watu, Je itakuwa ndoa? Wewe ukishasema mameno
rahisi; Kwa mfano; ‘nimeomba kwa muda, na hivi ndivyo ninavyosikia moyoni
mwangu kwamba, nakupenda sana, na ikiwa itampendeza Mungu na wewe pia, basi uwe
mwenzi wangu wamaisha’. Ukishamwambia maneno hayo rahisi (au yanayofanana na
hayo) amini kwamba kama ni mpango wa Mungu muwe wote maishani, maombi yako
na neema ya Mungu vitamsaidia kufanya uamuzi mzuri kwa ajili yenu wawili.
Unaweza kupata jibu la ‘ndiyo’ au ‘hapana’ au ‘subiri’. Mtu wa Mungu huongozwa
na Mungu, halazimishi wala hakasiriki ovyo kwa kitu kama hiki. Maana yangu ni
kwamba, hauhitaji kutumia nguu ya mwili wala akili (kuwaza sana). Baada ya
kuongea na kutua mzigo wako kwake, pumzika naumwachie Mungu kumalizia kazi.
Mkumbuke
Mariam mama wa Yesu, japo alijua ana mchumba, lakini malaika aliposema naye
kuhusu kupata ujauzito kabla ya ndoa, hakukurupuka mbio kwenda kwa Yusufu na
kuanza kumwelesha, bali alimwachia Mungu kuongea na Yusufu. Mimi binafsi
naamini Mariam alimwombea sana Yusufu. Lakini kwasababu ulikiwa mpango wa Mungu
wa kuwa pamoja maishani, Mungu hakuongea na Mariam peke yake; aliongea na
Yusifu pia. Mungu ni Mungu wa utaratibu, usimfundishe kazi. Jifunze kupumzika
ndani ya Mungu na kutokuwa na wasiwasi. Huko ndiko kukua kiroho. Amani ya Kristo
ikuhifadhi.
7.
Thibitisha uhusiano wako/wenu (kiofisi). (*Wimbo 3:4)
Baada
ya kuongea na kulitafakari pamoja kwa muda mtakaoona unatosha au unafaa, ni
muhimu sana sasa mpelekane mbele, katika mamlaka zenu za kifamilia na kikanisa.
Uhusiano mzuri usiwe wa mafichoni. Tunaona huyu mpenzi katika kitabu cha Wimbo
anasema, anataka kumtafuta mpenzi wake, amshike mkono, wapelekane kwa wazazi.
Huo ndio utaratibu mzuri kibiblia. Familia na kanisa watawasaidia kufuata
taratibu za kiutamaduni na kiroho ili mhalalishwe kuwa mume na mke. Ndipo ndugu
na marafiki mtawashirikisha mipango yote ili kuandaa harusi na makazi.
prepared
by JOSEPH JOACHIM
@SOKOINE
UNIVERSITY OF AGRICULTURE (TMCS-SUA)
josejoachim01@gmail.com
Who gives out agape love? Is it possible for we Christians practice this love one to another? When we love God which kind of love do we apply? Was Peter’s reply to Jesus that He knew that he loved Him an agape or other type of love? Please prove it through the Scriptures.
ReplyDeleteAmen mtumishi Mungu akuinue viwango na viwango kwa somo zuri
ReplyDeleteBlessings
ReplyDeleteAhsante Sana Mtumishi kwa SoMo zuri na Mungu azidi kukutumia katika kutufundisha vijana
ReplyDeleteAsante mtumishi
ReplyDelete